Jinsi ya kuuliza AI vizuri: mwongozo wa maagizo
Jibu baya mara nyingi linatokana na swali baya. Hizi ni sehemu nne za agizo linalofanya kazi.
Maagizo (prompti) ni maneno unayoandika kwa AI. Watu wengi wanaandika neno moja — "biashara" — kisha wanashangaa jibu ni la jumla. Agizo zuri lina sehemu nne.
1. Nani. Mwambie AI ianze wapi. "Wewe ni mwalimu wa hesabu wa kidato cha pili Tanzania."
2. Nini. Sema kazi haswa. "Nitengenezee maswali kumi ya mazoezi kuhusu asilimia."
3. Kwa ajili ya nani. Taja msomaji. "Kwa wanafunzi wanaosoma kwa Kiswahili, wenye umri wa miaka 14."
4. Umbo la jibu. Sema unataka jibu lije vipi. "Andika kila swali kwenye mstari mmoja, kisha weka majibu mwishoni."
Ukiunganisha: "Wewe ni mwalimu wa hesabu wa kidato cha pili Tanzania. Nitengenezee maswali kumi ya mazoezi kuhusu asilimia, kwa wanafunzi wenye umri wa miaka 14 wanaosoma kwa Kiswahili. Andika kila swali kwenye mstari mmoja, kisha weka majibu mwishoni."
Tofauti kati ya agizo hili na neno "hesabu" ni kubwa mno.
Mbinu tatu za ziada
- Mpe mfano. Kama unataka barua ya biashara, bandika barua moja uliyoandika zamani na useme: "Andika nyingine kama hii, lakini kwa mteja wa Mwanza."
- Mwambie asifanye nini. "Usitumie maneno ya kigeni. Usirefushe."
- Uliza tena. Jibu la kwanza ni rasimu. "Fupisha kwa nusu" au "Nipe njia nyingine tatu" hubadilisha kila kitu.
Onyo moja: AI haijui biashara yako, shule yako, wala kijiji chako. Ukitaka jibu linalokufaa, lazima uweke habari hizo kwenye agizo lako mwenyewe.
Habari zaidi
Tulijaribu: ChatGPT kwa Kiswahili
Kiswahili chake ni kizuri kwa maandishi ya kawaida, lakini kinateleza kwenye mambo ya Tanzania ya leo.
AlphaGenome Atlas: Ramani ya AI ya Kila Mabadiliko Yanayowezekana ya DNA
Google DeepMind imetoa hifadhi kubwa ya bure ya utabiri wa AI kuhusu mabadiliko yote ya herufi za DNA katika binadamu — kwa ajili ya watafiti, si watumiaji wa kawaida.
Biashara ndogo: njia tano za kutumia AI bila gharama
Si lazima ubadilishe biashara yako. Anza na kazi moja inayokuchosha kila wiki.